Elimu ya Chekechea imeimarishwa Nandi

Gavana wa Nandi, Stephen Sang, amesisitiza tena ahadi ya serikali yake ya kuimarisha elimu ya chekechea (ECDE), akisema kaunti hiyo itaendelea kuwekeza katika miundombinu na programu zinazolenga kuwapa watoto msingi imara wa kujifunza.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa darasa jipya la elimu ya watoto wadogo katika Kituo cha ECDE cha St. Thomas Kapkoros, Sang amesema elimu ya watoto wadogo ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo ya kaunti hiyo kwa sababu inaweka msingi ambao watoto hujengea elimu yao ya baadaye.

Gavana huyo amesema serikali ya kaunti imeweka kipaumbele katika ujenzi na uboreshaji wa madarasa ya ECDE kote kaunti ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata mazingira salama, ya kisasa na yanayofaa kwa ajili ya kujifunza.

Amesema kuwa uwekezaji katika sekta ya Elimu ya Chekechea haupaswi kuchukuliwa kama ujenzi wa madarasa pekee, bali kama uwekezaji wa muda mrefu katika rasilimali watu ya Kaunti.

Amedokeza kuwa kuwa serikali yake itaendelea kushirikiana na jamii kubaini maeneo yenye upungufu wa miundombinu ya ECDE na kuelekeza rasilimali ili kuziba mapungufu hayo.

Kulingana na Sang, kuboreshwa kwa miundombinu ya kujifunzia kutawapa watoto motisha ya kuhudhuria shule na wakati huo huo kuwapa walimu mazingira bora zaidi ya kufundishia.

Sang amewahimiza wazazi kuhakikisha kuwa watoto wote walio katika umri wa elimu ya awali (ECDE) wanandikishwa shuleni na kuhudhuria masomo mara kwa mara, akisisitiza kuwa ushiriki wa wazazi ni muhimu sana katika kuamua mafanikio ya programu za elimu ya chekechea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *