Spika wa bunge la kaunti ya Trans-Nzoia Joshua Werunga ameelezea kutoridhika kwake na utendakazi wa mwanakandarasi wa kuweka lami barabara ya Lessos-Kwanza-Kolongolo-Chepchoina eneo bunge la Kwanza.
Werunga sasa anamtaka waziri wa uchukuzi nchini James Macharia kuzuru eneo hilo la kutathmini hali ya mradi huo.
Akiongea wakati wa hafla ya kumlaki waziri wa maji ya unyunyuziaji maji Cecile Kariuki na mwenzake wa ugatuzi Eugene Wamalwa katika soko la Kolongolo, spika huyo wa kaunti ameelezea hofu yake kwamba huenda pesa za mlipa ushuru takriban bilioni mbili nukta sita zimetumika visivyo.
Amewahimiza maafisa kutoka idara husika kuendeleza ukaguzi wa mara kwa mara katika barabara hiyo ili kuhakikisha kuwa mwanakandarasi huyo anatekeleza kazi yake kwa mujibu wa viwango vinavyohitajika.
Barabara hiyo ya kilomita 63 inatarajiwa kuunganisha eneo hilo na kaunti ya pokot magharibi, kadhalika taifa jirani la Uganda baada ya kukamilika.