Serikali za Kaunti kusubiri zaidi

Serikali za kaunti zitalazimika kusubiri kwa muda mrefu kupokea mgao wa fedha kutoka kwa hazina kuu baada ya kamati maalum ya seneti iliyobuniwa kutafuta mwafaka kuhusu mfumo wa kugawa pesa za kaunti kufeli kutanzua suala hilo.

Kamati hiyo ya wanachama 12 imekuwa ikifanya vikao kwa siku kadhaa sasa katika harakati za kutafuta mwafaka kuhusiana na suala hilo ambalo limezua mgawanyiko wa maoni miongoni mwa maseneta.

Kulingana na duru za kuaminika kutokana na yanayojiri katika kamati hiyo, hazina kuu ya kitaifa imesalia kimya baada ya wanachama wa kamati hiyo kuwasilisha ombi la shilingi bilioni tisa zaidi.

Seneti ilikuwa imeratibiwa kuandaa kikao maalum hii leo lakini spika wa bunge hilo Ken Lusaka ametupilia mbali uwezekano wa kikao hicho ikizingatiwa mvutano uliopo. Kulingana na duru, kaunti ambazo   zingenufaika na mgao mkubwa katika mfumo wa tatu wa ugavi wa mapato, zimedinda kukubali mfumo mbadala kwa wazo kuwa sharti zipate mgao uliokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *