Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma Noordin Haji ameagiza kushtakiwa kwa Naibu Chansela wa chuo Kikuu cha Maasai Maasai Mary Walingo kwa madai ubadhifu wa pesa za chuo hicho.
Walingo ni miongoni mwa washukiwa watano ambao mkurugenzi mkuu wa mashtaka – DPP ameidhinisha washtakiwe kwa kufuja takriban shilingi milioni 177 za chuo hicho.
Kulingana na taarifa kutoka ofisi ya DPP Walingo atashtakiwa pamoja na Prof. Simon Kasaine Ole Seno (Makamu wa Naibu chansela anayesimamia hazina), Prof. John Almadi Obere ( Kaimu makamu wa naibu chansela aliyekuwa anasimamia masuala ya wanafunzi kati ya mwaka 2016 na 2019), Anaclet Biket Okumu (Afisa wa hazina) na Noor Hassan Abdi (dereva wa naibu chansela).
Katika taarifa yake DPP anasema kwamba uchunguzi umebaini kuwepo kwa mpango mahsusi kufyonza pesa za chuo hicho, amesema kwamba kuna ushahidi wa kutosha kuwafungulia mashtaka watano hao.
Uchunguzi umebaini kwamba Naibu Chansela aliagiza maafisa wa ngazi za chini katika idara ya hazina kuandika hundi kwa benki mbali mbali na kumpelekea aweke saini akiwa na makamu wake au maafisa wa hazina waliyokuwa na idhini kuagiza kutoa pesa kwa akaunti za chuo hicho.
Haji anasema kwamba hawakufuata utaratibu unaostahili na kwamba hundi hizo zilikuwa za kugharamia mahitaji bandia ya kujitungia huku lengo likiwa kufuja pesa.
