Watu wawili wa familia moja wamefariki na mmoja kunusurika katika kijiji cha Kipkenda, eneo la Keiyo Kaskazini, baada ya mawe kubingirika na kuangukia nyumba yao usiku wa kuamkia leo.
Mkasa huu unajiri siku mbili tu baada ya mkasa wa maporomoko ya ardhi kukumba eneo la Chesongoch, kaunti ya Elgeyo Marakwet, ambapo hadi sasa miili ya watu 26 imepatikana.
Tukio hilo limehusishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mengi ya kaunti hiyo.
Kulingana na wakazi wa eneo hilo, tukio hilo lilitokea baada ya mvua kubwa kunyesha kwa muda mrefu, hali iliyosababisha mawe kutoka mlimani na kubingirika hadi kwenye makazi ya watu.
Mamlaka za usalama pamoja na maafisa wa serikali katika kaunti hiyo sasa wanatoa wito kwa wakazi wanaoishi maeneo ya milimani kuhamia sehemu salama, ili kuepuka majanga zaidi kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.