RAIS RUTO:sitisheni mgomo

Rais William Ruto ametoa wito kwa walimu kusitisha mgomo wao uliokuwa umepangwa mwezi huu wakati shule zitakapofunguliwa kwa  muhula wa tatu akihaidi kushughulikia matakwa yao amewahakikishia walimu maslahi yao.

Akizungumza wakati wa hafla iliandaliwa alipoongoza makala ya 96 ya tamasha ya muziki kwa shule  na taasisi za elimu nchini katika Ikulu ndogo ya Eldoret,Rais ameweka bayana kuwa serikali imeanza mazungumzo na vyama vya walimu vya KUPPET na KNUT ili kuzuia mgomo wa kitaifa ulioitishwa na vyama hivyo hivi maajuzi.

Walimu wanataka Tume ya Kuwaajiri Walimu, TSC itekeleze kikamilifu nyongeza ya mshahara ya mwaka 2021-2025 kwa mujibu wa Mkataba wa Maelewano (CBA), kupewa bima ya matibabu na kuwasilishwa kwa makato yote ambayo yalitolewa kwenye mishahara ya walimu lakini hayajawasilishwa kwa zaidi ya mwaka mmoja uliopita miongoni mwa matakwa mengine.

Iwapo mgomo wa  walimu utaandaliwa kama ilivyopangwa, basi huenda ukawa tishio kwa mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE iliyoratibiwa kuanza mwezi Oktoba.

Mbali na KNUT na KUPPET, Chama cha Wafanyakazi wa Viwanja vya Ndege (KAWU) pia kimeitisha mgomo kuanzia Jumatatu wiki ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *