Serikali kupunguza matumizi yake katika mwaka wa kifedha wa 2020/2021

Wizara ya Fedha imetangaza katika hati ya kisera ya bajeti (Budget Policy Statement-BPS) Serikali inapanga kupunguza matumizi yake katika mwaka wa kifedha ujao unaoanza Julai 2020 kwa kiwango cha asilimia 23.6 ya jumla ya utajiri wa kitaifa (GDP) kutoka asilimia 26 mwaka huu wa kifedha.

Hatua hiyo ya kupunguza matumizi inalenga kuisaidia serikali kupunguza pengo katika bajeti kwa kupindi hicho hadi asilimia 4.9 ya GDP. Katika mwaka huu wa kifedha pengo katika bajeti ni asilimia 6.3 ya GDP.

Taarifa hiyo ambayo inayojadiliwa na kamati mbalimbali za bunge imesema kuwa Serikali inapanga kukopesha Sh bilioni 222.9 kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini kuziba pengo katika bajeti. Vilevile, inapanga kukopa Sh bilioni 345.1 kutoka mashirika ya kifedha kutoka nje.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imelaumiwa na raia kwa kukopa pesa nyingi zaidi tangu ilipoingia mamlakani mnamo 2013. Na mwishoni mwa mwaka 2019 ilipandisha kiwango cha fedha ambazo inaweza kukopa kutoka Sh trilioni 6 hadi Sh trilioni 9.

Kenya imekuwa ikikopa fedha nyingi kwa ajili ya kufadhili miradi ya ujenzi wa miundomsingi, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mombasa hadi Nairobi. Mradi huo uligharimu Sh bilioni 337 ambayo ilianza kulipwa mnamo Juni 2019.

Pengo katika bajeti ya kitaifa pia imesababishwa na hali kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) hufeli kutimiza kiwango cha ukusanyaji mapato kilichokusudiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *