Maafisa wa polisi mjini Eldoret wamewatia mbaroni Washukiwa watatu wa wizi wa kimabavu katika eneo la Mogombet katika wadi ya Kipkenyo kaunti ya Uasin Gishu usiku mbili tofauti.
Watatu hao Frank Kipruto 20,Caleb Walukhu 23 NA Titus Kipruto mwenye umri wa miaka 24 walinaswa na maafisa hao wakiwa na bunduki mbili za AK47 na wamekuwa wakiwahangaisha wenyeji katika kaunti ya Uasin Gishu.
Akithibitihsa haya kamanda wa polisi katika kaunti ya Uasin Gishu Ayub Gitonga Ali alisema kwamba maafisa wa polisi walifika kwenye nyumba ya mshukiwa mmoja kati yao Titus Kipruto na kupata risasi 4 kwenye paa la nyumba hiyo na walifika nyumbani kwa Frank Kipruto eneo la Segero na kupata risasi 4 zikiwa chini ya ghodoro lake.
Gitonga alisema kwamba maafisa wa polisi walielekea kwenye eneo la Milimani nyumbani kwa Solomon Kosgei kilomita nne kutoka eneo la Segero na kupata gari linaloaminika kutumika kwa wizi pamoja na sare za polisi na cheti bandia cha NTSA .
Aliongeza kwamba polisi wameanzisha uchunguzi kuhusiana na tukio hilo na pindi uchunguzi utakapokamilika washukiwa hao watafikishwa mahakamani na kuongeza kwamba washukiwa hao wataendelea kuzuliwa kwenye kituo cha polisi cha Central.