BIDHAA GHUSHI ZANASWA KERICHO

Maafisa wa polisi kaunti ya Kericho wamenasa bidhaa ghushi za vileo zenye thamani ya Sh316,000 katika kituo cha Brook viungani mwa mji wa Kericho.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Kericho Kamau Karungo, maafisa wa usalama waliokuwa wakishika doria walinasa gari aina ya Nissan Caravan kutoka Nakuru lililokuwa likisambaza pombe katika maeneo ya Kaunti ya Kericho.

Alisema polisi walifanikiwa kuwakamata dereva na kondakta wake ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani, wakati polisi wakiendelea na uchunguzi zaidi.

Kamishna huyo  wa Kaunti, akihutubia wanahabari nje ya Kituo cha Polisi cha Brooke, alisema gari hilo lilikuwa likisafirisha katoni 95 kila moja ikiwa na chupa 20 za bidhaa ya kileo kwa jina ‘Best,’ huku katoni 16 pekee zilipatikana na stempu halisi za ushuru za Mamlaka ya Ushuru ya Kenya.

Karungo alikuwa ameandamana na Naibu Kamishna wa Kaunti ya Kericho Mashariki Stephen Orinde na Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Riko Ngare.

Alisema tayari amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo kuhakikisha kuwa hakuna pombe inayosambazwa usiku katika Kaunti Ndogo zote sita za Kericho akiwaonya wafanyabiashara wasio waaminifu kwamba siku zao zimehesabiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *