Arobaini za Mgema zatimia

Idara ya usalama ikishirikiana na washikadau mbalimbali katika Kaunti ya Uasin Gishu jumatatu ilizidisha  msako dhidi ya pombe haramu, na kuwakamata washukiwa wawili wakiwa na bidhaa ya ethanol yenye thamani ya takriban Sh1.25 milioni katika Kaunti Ndogo ya Kapseret.

Akiongea na wanahabari katika kituo cha  Polisi cha Langas, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Uasin Gishu Benjamin Mwanthi alisema shehena hiyo iliyonaswa ilikuwa na uwezo wa kubeba takriban lita 810 na ilikuwa ikisafirishwa kwa gari la kibinafsi.

Alithibitisha kuwa mwanamume na mwanamke wa makamo walikamatwa kuhusiana na shehena hiyo haramu.

Washukiwa hao wawili kwa sasa wako chini ya ulinzi wa polisi wakitarajiwa kufikishwa mahakamani.

Kulingana na uchunguzi wa awali, washukiwa hao walikuwa wamesafiri kutoka Kaunti ya Nandi hadi Uasin Gishu na wanaaminika kuwa walikuwa wakielekea Nairobi wakati wa kukamatwa kwao.

Mwanthi amebainisha kuwa kunasa huko kunafuatia operesheni sawia iliyoendeshwa wiki mbili zilizopita ambapo maafisa walinasa mitungi 31 ya chang’aa kutoka kwa gari lililokuwa likitoka Bungoma kuelekea Eldoret. Aliongeza kuwa kesi ya awali tayari iko mahakamani.

Mwanthi alisisitiza kuwa pombe haramu inaendelea kuhatarisha afya, kijamii na kiuchumi ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha kutokana na unywaji wa vitu vyenye madhara.

Alidokeza kwamba mashirika ya usalama yanashirikiana kwa karibu na washirika wakuu, ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Ushuru nchini (KRA) na Shirika la kukadiria ubora wa bidhaa nchini (KEBS) ili kukomesha biashara hiyo haramu.

Mkurugenzi wa Bodi ya Kudhibiti Vileo Kaunti ya Uasin Gishu (ADCB) Koiya arap Maiyo alipongeza juhudi zilizoratibiwa za timu ya mashirika mbalimbali, akihusisha ufanisi wa operesheni hiyo na ushirikishwaji mzuri wa ujasusi miongoni mwa mashirika ya usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *