Naibu gavana wa kaunti ya Uasin Gishu Evans Kapkea amepuuzilia mbali taarifa zinazodai kuwa kumekuwepo na tofauti baina yake na gavana wa kaunti hiyo Jonathan Bii Chelilim.
Awali kumekuwepo na taarifa zilizodai kuwa tofauti kati ya wawili hao, umekuwa kwa muda huku njama ya kuwasilisha hoja ya kumtimua naibu huyo kupitia kura ya kutokuwa na imani naye, ikiwa tayari na kuwa ingewasilishwa bungeni hivi karibuni.
Kapkea amepuuza madai hayo akisema kuwa kamwe hatojiuzulu na kuwa uhusiano kati yake na gavana Bii uko imara, akisema kuwa wamekuwa wakishirikiana katika utendakazi ili kuboresha maisha ya wakaazi wa kaunti ya Uasin Gishu.
Amesema kuwa uvumi huo unaenezwa na mahasimu wao kisiasa pamoja wale wasiotaka kuwepo kwa ufanisi katika kaunti ya Uasin gishu.