Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira inayoadhimishwa kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili watu wawe na uzima tele Rej. Yn 10:10. Zawadi hii ya uzima ndicho kiini cha utume na wito wa pamoja wa wanafunzi wa Kristo Yesu wa kujenga na kudumisha ustaarabu wa upendo.
Na Padre Richard A. Mjigwa C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa kuanzia tarehe 1 Septemba 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Hii ni ahadi ya amani kuu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambapo watu wataacha vita na ghasia na kutumia vyombo vya silaha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Itakumbukwa kwamba, siku hii ilianzishwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 10 Agosti 2015, kama sehemu ya mchakato endelevu na fungamani wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, 2015-2016. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume kuhusu utunzaji bora wa mazingira, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya Utunzaji wa Nyumba ya Wote anasema, mazingira ni kito cha thamani kwa ajili ya wote na kwamba, mazingira yana uhusiano wa pekee na maisha ya binadamu. Ongezeko la kiwango cha joto duniani linaendelea kusababisha ongezeko la kina cha maji ya bahari; ukame na mafuriko; dhoruba pamoja na majanga asilia. Hapa mwanadamu anahamasishwa kubadili mtindo wa maisha na maendeleo, kwa kuambata teknolojia rafiki kwa mazingira. Madhara ya mabadiliko ya tabianchi anasema Baba Mtakatifu Francisko yamepelekea baadhi ya watu kutumbukizwa katika utamaduni wa kutopea kwa imani, kutukuzwa kwa malimwengu na ubaridi wa imani mambo yanayoendelea kusababisha baadhi ya watu kutumbukizwa katika utumwa mamboleo na kazi za suluba; tatizo la kuwatelekeza wazee na kuwanyanyasa watoto, kwa mafao ya mtu binafsi.
Maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kundi ambalo linaathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa ni kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mapambano dhidi ya umaskini; kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani, haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa. Baba Mtakatifu Francisko aliwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha kazi ya uumbaji. Kwa kuthamini na kujali umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, maadhimisho haya yakachukua mfumo wa kiekumene na kilele chake ni hapo tarehe 4 Oktoba ya kila mwaka. Hii ni Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hiki ni kipindi muafaka cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa ya uumbaji, ni kipindi cha toba na wongofu wa kiikolojia sanjari na kujibu kwa vitendo kilio cha Mama Dunia na Maskini, hawa ndio wale “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.”
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa Siku ya 12 ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira kwa upande wa Kanisa Katoliki inayoadhimishwa kuanzia tarehe 1 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba 2026 unanogeshwa na kauli mbiu: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu.” Isa 2:4. Kristo Yesu alikuja ulimwenguni ili watu wawe na uzima tele Rej. Yn 10:10. Zawadi hii ya uzima wa milele ndicho kiini cha utume na wito wa pamoja wa wanafunzi wa Kristo Yesu wa kujenga na kudumisha ustaarabu wa upendo. Mama Kanisa anapoadhimisha Siku hii ya Kimataifa ya Kuombea Utunzaji Bora wa Kazi ya uumbaji, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaalikwa tena kutafakari juu ya zawadi ya maisha ya uzima na kuithamini dunia inayouendeleza, kwani hizi njia muafaka za kumtolea Mwenyezi Mungu sifa na shukrani. Leo hii, binadamu anashuhudia majanga mengi na mateso makubwa kwa binadamu, kuvurugika kwa kazi ya uumbaji nako kunaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa na kwamba, changamoto kubwa mbele ya binadamu ni kuomba uponyaji na amani inayopata chimbuko lake katika Ulimwengu uliojeruhiwa na kwamba, Mungu wa uzima aliyefunuliwa na Kristo Yesu ndiye kiini cha amani hii ambayo kamwe Ulimwengu hauwezi kuitoa: “Amani nawaachia; amani yangu nawapa” Yn 14:27. Hii ni amani inayobubujika kutoka katika upendo wa kudumu wa Kristo Yesu na utunzaji wake kwa kila mwanadamu.
