Polisi wakwama na maiti ulioharibika Eldoret

Polisi walikwama wakiwa na mwili ulioharibika katika kituo chao na kwenye gari baada ya vyumba vitatu vya kuhifadhia maiti kukataa kuupokea katika kaunti ya Uasin Gishu maafisa wa vyumba hivyo wakitaja ukosefu wa nafasi.

Mwili huo ulipatikana kutoka Bwawa la Mugoya katika kaunti ndogo ya Soy, kaunti ya Uasin Gishu.

Kisa hicho kiliripotiwa Juni 16 baada ya mwanamume aliyekuwa akichunga kondoo wake kuuona ukielea kwenye bwawa hilo.

Maafisa wa polisi walitembelea eneo la tukio na kuthibitisha mwili huo ulikuwa ukielea ndani ya maji na maafisa wa kikosi cha zima moto kutoka kaunti ya Uasin Gishu wakauchukua.

Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa marehemu alikuwa mwanaume Mwafrika asiyejulikana mwenye umri wa miaka 35 hivi na mwili wake ulikuwa umeanza kuoza.

Maafisa wa kushughulikia maeneo ya uhalifu walifika eneo hilo na kuchukua maelezo muhimu kwa ajili ya uchunguzi.

Mwili huo ulizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kamukunji ukisubiri taratibu za kuingizwa katika chumba cha kuhifadhia maiti huku uchunguzi ukiendelea kubaini utambulisho wa marehemu na chanzo cha kifo.

Polisi walisema mwili huo baadaye ulipelekwa katika hifadhi moja ya maiti ya eneo hilo hiyo jana Jumatano kufuatia uingiliaji kati.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *