Baba Mtakatifu Leo wa XIV ametoa onyo kali kwa wasafirishaji haramu wa binadamu na wengine wanaonufaika kutokana na mateso ya wahamiaji na ya kibinadamu kutubu.
Katika mkutano na wahamiaji pamoja na wafanyakazi wa huduma za ujumuishaji wa kijamii huko Plaza del Cristo de La Laguna, wakati wa ziara yake katika Visiwa vya Canary nchini Uhispania, Papa Leo alisema fedha zinazopatikana kwa kutumia udhaifu wa maskini hazitaleta amani, heshima wala maendeleo.
Papa Leo amesema alitaka kutuma ujumbe wa wazi kwa wale wanaotumia vibaya hali ya kukata tamaa kwa wengine; wanaopanga njia za mauti, wanaojihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu, wanaonyang’anya watu hati zao, wanaowanyanyasa wafanyakazi, kuwatishia wanawake, kudanganya familia na kugeuza mateso ya wengine kuwa biashara.
Mapema, wahamiaji walimueleza kiongozi huyo wa kiroho changamoto wanazopitia.
Wakati huo,Papa Leo amesisitiza kuwa Kristo Yesu,Mwana wa Mungu anaona madonda ya vita kinzani na migogoro sehemu mbalimbali za maisha ya mwanadamu,anauona utupu wa maisha ya mwanadamu unaokita mizizi yake katika ulaji wa kupindukia. Amewataka wanadamu kutoweka nyuso za bandia, na kuhakikisha familia zao hazigubikwi na migogoro, na kwa vijana kuwa na mwelekeo ulio bora maishani mwao.
