HOMABAY; WAKAAZI WAHAMASISHWA KUHUSU EBOLA

Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kwa kushirikiana na serikali ya Kaunti ya Homa Bay wameanza kutoa mafunzo kwa washikadau mbalimbali ndani ya kaunti hio ili kuwafahamisha kuhusu Virusi vya Ebola.

Viongozi wa jumuiya hiyo walitolewa kutoka kaunti ndogo nne zinazopakana na Uganda zikiwemo Suba Kaskazini, Suba Kusini, Suba ya Kati na Homa Bay Town.

Mafunzo hayo yaliyofanyika hio jana ndani ya mji wa Homa Bay yamewaleta pamoja viongozi wakiwemo machifu, viongozi wa vijana, wenyeviti wa sekta ya bodaboda, viongozi wa kidini, wenyeviti wa Kitengo cha Usimamizi wa Ufuo miongoni mwa wengine kutoka Kaunti Ndogo nne.

Hii ni baada ya takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kubainisha kuwa hadi kufikia Novemba 22 mwaka huu, visa 141 za ugonjwa wa Ebola (EVD) vilithibitishwa duniani, ikiwa ni pamoja na vifo 55 (case fatality rate (CFR): 39%).

Nchini Uganda jumla ya visa 36 ikiwa ni pamoja na 18 zilizothibitishwa na visa 18 zinazowezekana na vifo 23 (CFR 64%) viliripotiwa kufikia Septemba 25.

Hofu ya virusi hivyo kufikia kaunti ndogo hizi nne ambazo ziko kando ya Ziwa Victoria imechochea maandalizi ya sasa katika mikoa hii.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mratibu wa Msalaba Mwekundu Kaunti ya Homa Bay, Samuel Omondi aliwataka washikadau hao kuripoti kisa chochote kinachoshukiwa kwa matibabu ya awali na kutengwa ili kudhibiti virusi.

Kutokana na hali ya kuambukiza ya ugonjwa huo Omondi aliwaonya wafunzwa kuepuka kabisa kuwasiliana na watu wanaoshukiwa bila vifaa vya kujikinga.

Afisa wa Ukuzaji Afya wa Kaunti Ndogo ya Suba Kusini, Kennedy Amayo alisema kuwa wakaazi wanaoishi katika kaunti ndogo nne wako katika hatari kubwa ya kuambukizwa virusi hivyo kutokana na shughuli za biashara za kuvuka mipaka.

Amayo aliwataka wakazi hao kuwa waangalifu kila wanapokutana na wageni kutoka Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanaofanya biashara kwenye fukwe hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *