Mbunge wa Keiyo Kaskazini, Adams Kipsanai, amewataka wakazi wa eneo bunge hilo hasa wale ambao bado hawajajisajili katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kufanya hivyo ili kuepuka mahangaiko wanapotafuta huduma za matibabu.
Wito huu unajiri huku kukiwa na ripoti kwamba idadi kubwa ya wakazi bado hawajajisajili kwenye mpango huo wa afya.
Akizungumza katika eneo la Salaba katika eneo la Keiyo Kaskazini, Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Kipsanai amesisitiza umuhimu wa kuwa na bima ya afya, akisema kuwa inatoa usalama muhimu wakati wa dharura za matibabu.
Wakati uo huo, Mbunge huyo amedokeza kuwa Rais tayari amewasilisha pendekezo katika Bunge la Kitaifa ili kujumuisha kipengele maalum cha kutenga fedha kutoka kwa hazina ya NG-CDF.
Mpango huu unalenga kuiwezesha serikali kugharamia bima ya afya kwa wananchi wasiojiweza ambao hawana uwezo wa kifedha wa kujiandikisha au kujilipia bima hiyo wenyewe.
