Kanisa katoliki nchini limetupilia mbali divai ambayo imekuwa ikitumika katika misa takatifu, na kuzindua divai nyingine mpya itakayotumika kwenye maadhimisho ya kiliturjia.
Mwenyekiti wa Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB Maurice Muhatia Makumba, amesema kuwa baraza hilo limesitisha matumizi ya divai hiyo kwenye misa takatifu, kwa kuwa imekuwa ikitumika visivyo na wale wasio waumini wa kanisa katoliki, na kutoa amri kuwa divai hiyo kamwe isitumike katika misa takatifu.
Askofu Muhatia amesema kuwa divai itakayotumika kwa sasa ina nembo ya baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB, na sahihi ya mwenyekiti wa baraza hilo, akitoa wito kwa kila jimbo kuweka mikakati na sheria dhabiti, itakayoongoza ununuzi wa divai hiyo katika majimbo yao ili isitumike visivyo.
Ametoa wito kwa wakristu kadhalika kutonunua divai ambayo imekuwa ikitumika hapo awali, kwa lengo la kuleta kanisani kama zawadi.
Hata hivyo askofu mkuu Muhatia amesema kuwa majimbo mbalimbali tayari yameweka tarehe rasmi ya kuacha kutumia divai hiyo, akitoa wito kwa kila mmoja kuwa mwangalifu, ili divai hiyo mpya isiingie mikononi mwa wale hawajaruhusiwa kuitumia.