Baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB limetoa wito wa Amani na maridhiano haswa wakati huu ambapo taifa linapitia changamoto nyingi.
Akihubiri katika misa ya kuombea taifa iliyoandaliwa katika eneo la sala la Maria Subukia jimbo katoliki la Nakuru, askofu wa jimbo katoliki la Embu Peter Kimani Ndungu, ametoa wito kwa viongozi kukaza Kamba kwa faida ya umoja na maridhiano katika taifa, akisema kuwa umoja huo ndio utakaoleta ufanisi nchini.
Naye mwenyekiti wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini KCCB Maurice Muhatia Makumba, amesema kuwa vijana wengi nchini kwa Sasa wanapitia changamoto si haba, zikiwemo msongo wa mawazo, ukosefu wa ajira, wimbi la tabia kutoka kwa mataifa ya magharibi miongoni mwa mengine, akiwataka siku zote kutafuta hifadhi kwa kanisa, na viongozi wa kidini kama njia moja ya kupata ushauri nasaha na malezi ya kiroho.
Baraza Hilo kadhalika limetoa wito kwa vijana kamwe kutokubali kupotoshwa na Mila za kigeni kama vile ndoa ya jinsia Moja almaarufu LGBTQ, likisema kuwa hulka hiyo Haina nafasi nchini na inakwenda kinyume na mafunzo ya kanisa pamoja na itikadi za afrika.
Askofu Muhatia kadhalika amewataka vijana kuwa kwenye msitari wa mbele wa kuleta mageuzi nchini, wakijitosa katika pambano dhidi ya jinamizi la ufisadi, akiwataka kamwe kutokubali kutumika na wanasiasa kuzua vurugu nchini