Askofu wa jimbo katoliki la Eldoret Dominic Kimengich ametoa wito kwa wakenya kuishi pamoja na upendo pasi na kubagua yeyote kwa msingi wa ukabila, akisema kuwa upendo huo una uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi nchini.
Akihubiri katika misa ya krismasi kwenya kanisa la Moyo mtakatifu wa Yesu Kathedrali, askofu Kimengich ametoa wito kwa kila mmoja kuonyesha amri kuu ya Mungu ya upendo kwa wenzao, kwa kuwa taifa ambalo limejawa na upendo huafikia kwa urahisi miradi ya maendeleo na mshikamano wa kitaifa.
Askofu Kimengich kadhalika ametoa wito kwa kila mmoja kumkaribia kristu kwa kuwa yeye ndiyo atakayewapa nguvu na matumaini ya kukabiliana na changanmoto mbalimbli ibuka.
Wito sawia na huo umetolewa na askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Nairobi Philip Anyolo, ambaye ametoa wito kwa wakenya kuendelea kudumisha Amani na umoja licha ya hali ngumu ya maisha, akisema kuwa umoja huo ndio utakaokwamua visa vingi ambavyo vinaathiri shughuli za maendeleo nchini vikiwemo ufisadi.
