Mwezi Oktoba 2025,Kanisa Katoliki nchini Papua New Guinea litashuhudia tukio la kihistoria.Mama Kanisa atamtangaza Mwenyeheri Peter To Rot,aliyekuwa Katekista mnyenyekevu,mume na baba,kuwa Mtakatifu wa kwanza wa Taifa hilo.
Katika kuelekea siku ya kutangazwa kwa Mwenyeheri wa Papua New Guinea hivi karibuni, mwezi wa kumi Radio Vatican, ilimfikia kwa njia ya Simu na kuzungumza na Padre Tomas Ravaioli, mmisionari kutoka Argentina ambaye amehudumu Papua New Guinea kwa miaka 15 na Makamu wa mchakato wa kutangazwa Mtakatifu kwa Mwenyeheri Peter To Rot. Katika maoni yake, Mmisionari huyo alisema, “Watu hapa wanafuraha sana. Yote yametokea haraka, na hii ni kama zawadi ya mwisho ya Papa Francisko kwa nchi yetu. Hatujawahi kuwa na Mtakatifu, na mwezi ujao tutapata Mtakatifu wa kwetu wa kwanza.”
Peter To Rot alizaliwa mwaka 1912 alikuwa mtoto wa chifu wa Kijiji cha Rakunai, Papua New Guinea. Alikuwa baba wa watoto watatu, na zaidi ya yote, mwenye imani aliyeishi maisha ya kawaida lakini yenye mizizi ya kina katika imani ya Kikristo. Peter To Rot aliishi maisha yaliyojaa imani thabiti. Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, wamisionari walipofungwa gerezani, yeye alichukua jukumu la kichungaji: akifundisha watoto katekisimu, kuwaandaa wanandoa katika sakramenti ya ndoa, na kupeleka Ekaristi Takatifu kwa siri, mara nyingi akitembea kwa saa nyingi licha ya upinzani wa utawala wa Kijapani.