KEMRI kuanzisha kituo kipya kaunti ya Uasin Gishu

Maafisa kutoka KEMRI na wenzao kutoka kaunti ya Uasin Gishu

Taasisi ya Utafiti wa Matibabu nchini, (KEMRI) inatazamiwa kuanzisha kituo kipya cha utafiti katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Akiongea katika Makao Makuu ya Kaunti hiyo wakati wa ziara yake, mwenyekiti wa Bodi ya KEMRI, Dkt. Abdullahi Ali alifichua kuwa bajeti tayari imetengwa ili kuhakikisha kuwa kituo cha utafiti kinaanzishwa mara moja hapa mjini Eldoret.

Katibu wa kaunti ya Uasin Gishu Edwin Bett aliyepokea ujumbe huo kwa niaba ya gavana Jonathan Bii, aliwahakikishia kuwa serikali ya kaunti hiyo chini ya uongozi wa gavana Chelilim, iko tayari kutoa ardhi kwa ajili ya kuanzishwa kwa kituo hicho cha utafiti kwa manufaa ya wakazi.

Waziri wa Ardhi, Mipango, Makazi na Maendeleo ya Miji wa kaunti hiyo Dkt. Janeth Kosgei, aliongoza timu hiyo katika ziara ya kutembelea sehemu nne za ardhi ya umma kwa ajili ya KEMRI kutambua sehemu inayofaa zaidi kwa mradi huo.

Mwenzake wa Huduma za Afya kwenye kaunti hiyo Abraham Serem, alishukuru mpango huo akibainisha faida zitakazokuja pamoja na kituo cha utafiti zitakuwa na manufaa kwa wakazi, akibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo utajumuisha ujenzi wa kituo cha afya ndani ya taasisi ya utafiti.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *