Ipo haja ya familia changa kuwa na hulka ya kusemezana kila kuchao kama njia moja ya kufanikisha mshikamano baina yao na hata kupiga jeki swala la malezi.
Haya ni kwa mujibu wa askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Nairobi Philip Subira Anyolo kwenye misa ya kipaimara kwenye kanisa ya st Mary Mother of God Githurai jimbo kuu katoliki la Nairobi akisema kuwa swala la malezi linashirikisha wanandoa wote na hivyo wanastahili kushauriana kila wakati, akihoji kuwa familia nyingi husambaratika kutokana na ukosefu wa kusemezana kila wakati.
Alitoa wito kwa familia zilizochini ya miaka hamsini kwenye ndoa kumakinikia mashauriano kila wakati kwa kuwa ni katika umri huo ndio kunakuwa na changamoto nyingi ambayo mara nyingi huzua uhasana miongoni mwa jamii.
Aliwataka wakristu kujitwika jukumu la kuishi maisha ya sakramenti akisema kuwa sakramenti ni mwanga na tija ya kuwezesha kile ambacho kinaonekana kuwa ngumu kuwa rahisi katika familia.