Ripoti mpya inaonyesha kuwa Wakenya wanaviamini vyombo vya habari kuliko wanavyoiamini serikali.
Ripoti ya mwaka huu kuhusu hali ya vyombo vya habari imeonyesha kwamba imani ya wakenya wengi kwa vyombo vya habari imeongezeka kutoka asilimia 94 hadi asilimia 97 mwaka huu huku runinga na redio zikitumika sana kwa habari.
Ripoti hiyo imetolewa na baraza la vyombo vya habari mjini naivasha siku ya ijumaa. Katika utafiti uliofanywa na Infotrak Research and Consulting, Zaidi ya watu 3000 walihojiwa kuhusu utendakazi wa vyombo vya habari .
Afisa mkuu mtendaji wa baraza hilo David Omwoyo amesema wakati serikali ilipopiga marufuku usafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine, watu wengi walitegema vyombo vya habari kufahamu yaliokuwa yakifanyika hasa kwa wale ambao hawakuweza kupata huduma za mitandao. Mwenyekiti wa baraza hilo Maina Muiruri amesema janga la corona liliathiri sana sekta ya habari na kusababisha kupungua kabisa kwa mapato yake na kupelekea watu wengi kupoteza kazi zao au kupunguzwa mishahara. Hata hivyo ameonyesha matumaini kwamba mambo yataboreka katika miezi kadhaa ijayo.